Jumatano, 18 Desemba 2019

MAMBO YANAYOATHIRI MAWASILIANO YA WATU KATIKA JAMII:

 ðŸŽ“Jamii-lugha yoyote, yaani kundi la watu linalotumia au kuzungumza lugha ya aina moja, limekubaliana kuwa lugha haitumiki kiholela bali matumizi ya lugha hudhibitiwa na mambo fulani. Haya ndiyo tunayoita kaida za matumizi ya lugha.

👉 Kaida ni kanuni au sheria ambazo hazikuandikwa.

👉Hii ni kumaanisha kuwa jamii-lugha zimekubaliana kuwa matumizi ya lugha hudhibitiwa na kanuni hizi. Kaida(kanuni) zenyewe ni zifuatazo:

✍Umri

Jamii-lugha zote zimekubaliana kuwa matumizi ya lugha huimarika kutegemea ongezeko la umri wa watu. Hii ndiyo sababu matumizi ya lugha ya mzee yanatarajiwa kusheheni tamathali nyingi za semi katika lugha. Wazee wanatarajiwa kuwa wanapozungumza, hawabwagi mambo kama vile vijana wafanyavyo bali huyagubika kwa mafumbo na tauria. Vijana kwa kawaida hawajali uteuzi wa maneno wanayotumia na zaidi hupenda kutumia lugha isiyo sanifu.

✍Wahusika na uhusiano wao

Matumizi ya lugha pia hutawaliwa na wahusika wanaoshiriki mazungumzo pamoja na uhusiano wao. Bila shaka, tukisikiliza mazungumzo yoyote yale, tunaweza kung’amua wahusika wana uhusiano gani. Mathalani, mazungumzo ya mahirimu yatasheheni matumizi ya lugha yenye utani, mzaha au maneno yenye ukali ilhali wahusika hawatiani magumi bali ni kuchangamka. Hiki ni kinyume cha matumizi ya lugha baina ya mzazi na mwanawe, au mtu na mkubwa wake kazini, ambapo matumizi ya lugha yatadhihirisha unyenyekevu na heshima.Maungumzo kati ya watu ambao wana uhusiano rasmi, kwa mfano, daktari na mgonjwa au hakimu na mshukiwa watatumia lugha yenye heshima na urasmi mwingi.Watu ambao hawafahamiani pia watatumia lugha kwa njia ya kipekee wakilinganishwa na wale ambao wanafahamiana. Kwa ujumla, sifa za matumizi ya lugha kati ya watumiaji tofauti vile vile ni tofauti.

✍Muktadha wa kihali

Matumizi ya lugha vilevili hutegemea hali ambamo mtu anajipata. Je, hali iliyoko ni ya furaha au majonzi? Je, watu wanasherehekea ama wana matanga? Je, ni hafla ya aina gani na ni msamiati wa aina gani ambao utafaa kutumiwa katika muktadha huo? Kufahamu hali iliyoko inasaidia kuteua msamiati wa kutumia.

✍Madhumuni au lengo

Lugha inapotumiwa huwa inalenga jambo fulani. Haya ndiyo madhumuni ambayo hudhibiti namna tunavyotumia lugha. Mazungumzo yanaweza kulenga kushutumu, kukashifu, kushauri, kunasihi na kadhalika. Malengo haya huhitaji lugha itumike kwa namna ambavyo lengo litaafikiwa. Nayo huhitaji wahusika katika mazungumzo kuteua msamiati unaochukuana na madhumuni ya mazungumzo hayo. Mathalani, iwapo anataka kuvutia msikilizaji, kama vile kasisi anapohubiri, lugha yake itakuwa na unyenyekevu na ushawishi kwa mpokezi.

✍Hadhi au cheo cha mtu

Cheo au madaraka hutarajiwa kuathiri matumizi ya lugha ya anayehusika. Hakimu mahakamani, mwalimu shuleni, kasisi kanisani, imamu msikitini na kadhalika sharti wateue maneno kulingana na mamlaka au vyeo vyao. Aidha, tofauti katika vyeo pia huathiri matumizi ya lugha. Watu ambao wana cheo kimoja hutumia lugha bila urasmi mkubwa huku watu walio katika vyeo tofauti wakitumia urasmi mwingi. Kwa mfano, mfanyikazi ambaye atazungumza na meneja ama msimamizi wake huenda atumie lugha ambayo ni rasmi maana atakuwa anazungumza na mkubwa wake na shughuli zitakuwa rasmi. Hata hivyo, mfanyikazi akikutana na mwenzake ambaye wanafanya naye kazi afisi moja na cheo chao ni sawa, watatumia lugha ya utambulisho Fulani.

✍Jinsia/ uana

Takriban katika jamii-lugha zote, pana tofauti kubwa za matumizi ya lugha ya kawaida baina ya jinsia ya kike na ya kiume. Mathalani, tutapata kuwa matumizi ya lugha ya jinsia ya kike husheheni vihisishi vingi kuliko jinsia ya kiume. Aidha, matumizi ya lugha ya jinsia ya kike hudhihirisha kuwa na tauria au tasfida Zaidi kuliko yale ya jinsia ya kiume. Aghalabu wanapoongea, wanawake hufunikafunika mambo ya siri au yenye ukali mwingi kuliko wanaume. Wanaume mara nyingi huyabwaga mambo bila ya kuyatafutia tafsida. Aidha, wanaume hutumia lugha tofauti na wanawake wanapozungumza kati yao au kati ya mwanamke na mwanamume.

✍Aina ya tungo

Tungo mbalimbali hujibainisha kwa matumizi mahsusi ya lugha. Kwa mfano:

Mazungumzo – yatatumia kauli fupifupi kati ya wahusuka.

Barua rasmi – lugha rasmi ambayo haina ufafanuzi ama maelezo mengi.

✍Malezi

Malezi ya mtu nayo yana nafasi kubwa katika kudhibiti matumizi yake ya lugha. Haya hutegemea Zaidi mtu amezalika katika familia ya aina gani. Kuna familia ambapo mtoto hana uhuru wa kunena kwa namna yoyote mbele ya watu wazima. Endapo mtoto atasema chochote, ni pale tu ambapo ameulizwa swali na anatarajiwa kulijibu. Anapojibu, anatakiwa kutoa jibu fupi sana. Hali hii humwathiri mtoto kama huyu kwani hukosa kuingiliana na kustawisha stadi zote za lugha kikamilifu. Aghalabu watu kama hawa watatambulikana katika utu uzima wao kwa haiba ya undani (introvert). Malezi waliyoyapata yaliwaathiri katika matumizi ya lugha. Hawa ndio watu ambao hawachangii lolote katika tukio ambapo watu wanazungumza. Endapo watasema jambo, ni pale ambapo swali limewalenga wao wenyewe na hawawezi kuepuka. Hata hivyo, watalijibu kwa ufupi na kunyamaza.

✍Tabaka

Mara nyingi jamii-lugha inaweza kugawika katika matabaka kutegemea uwezo wa kiuchumi. Mgawiko huu hufanya tabaka fulani kujitengea eneo fulani kama makaazi yake. Tukichunguza matumizi ya lugha katika eneo linamoishi kila tabaka, tutatambua kuwa kuna tofauti kubwa sana. Tofauti hizi zinatokana na mgawiko huu. Mathalani, katika matabaka ya chini ambayo ni ya wachochole, aghalabu hali hii ya maisha huwafanya wanatabaka hawa kukosa vidhibiti ulimi wanapotumia lugha. Katika makaazi yao, si ajabu kusikia maneno mazito kama vile shetani, mbwa, nugu, malaya na kadhalika yakitumika kila dakika kwa kurejelea mtu. Hali hii haipatikani kwa wepesi katika maeneo ya mabwanyenye. Endapo shetani atatajwa katika sehemu hii, ni pale maabadini au wakati wa kumrejelea ibilisi wala si mtu. Vivyo hivyo, mbwa atatajwa kwa kumrejelea mnyama mwenyewe wala si mtu. Hata hivyo, lugha ya hawa ‘waliostaarabika’ huweza kuashiria kiburi kiasi Fulani maana inakuwa na kujivuna kutokana na uwezo wa jamii waliomo – labda gari la kifahari, jumba mithili ya kasri, biashara kubwa na kadhalika.

✍Idadi ya lugha azijuazo mtu

Idadi ya lugha katika jamii na uwezo wa wahusika katika kutumia lugha hizo ni jambo jingine linalodhibiti matumizi ya lugha. Iwapo lugha zinazotumika ni zaidi ya moja na wahusika wana uwezo wa kuzitumia, moja kwa moja patatokea hali ya kuchanganya ndimi au msimbo, na vilevile kubadilisha ndimi au msimbo. Ujuzi wa lugha azijuazo mzungumzaji huzusha kuchanganya ndimi iwapo mzungumzaji hana ufasaha wa kutosha katika lugha anayoitumia.

✍Hali ya mtu

Hii ni kaida nyingine ambayo hudhibiti matumizi ya lugha. Hali inayoibusha hisia kama za hamaki humfanya mtu kusema jambo ambalo atakuja kujijutia baadaye. Hii ndiyo sababu methali zimezuliwa kuelezea matokeo ya hasira na kuwatahadharisha wanajamii dhidi ya kuzungumza au kufanya jambo katika hali ya hasira. Methali Hasira hasara au Hasira za mkizi, tijana ya mvuvi hutumika kuelezea hali hii.

Matumizi ya lugha pia yatategemea iwapo mzungumzaji yu mgonjwa, mlevi, mchangamfu, mwenye furaha, mwenye huzuni. Kwa mgonjwa hutumiwa lugha ya kuliwaza na yenye huruma. Mlevi naye hutumia lugha ovyo bila kuzingatia matumizi ya lugha ya adabu.

✍Muktadha au mazingira

Muktadha au mazingira ambamo mazungumzo hutokea huwa na nafasi kubwa sana katika kudhibiti matumizi ya lugha. Watu hutumia lugha kulingana na muktadha au mazigira waliyomo. Iwapo mazungumzo yanatokea ofisini au mazingira mengine rasmi, basi lugha itakayotumika ni ya heshima na pia yenye urasmi. Iwapo mazungumzo yanatokea mitaani au nyumbani, basi kiwango cha urasmi kitapungua.Aghalabu mazungumzo ya mtaani au nyumbani hutumia lugha isiyo rasmi. Katika kiwango cha msamiati, mabadiliko hutokea kutoka mahali pamoja hadi pengine.Kwa mfano, msamiati wa hospitali ni tofauti na ule wa mahakamani au maabadini.

✍Mada au yaliyomo katika mazungumzo

Mada ni muhimu sana katika uamuzi wa namna ya kutumia lugha. Kwa mfano, ikiwa mada inayozungumziwa inahusu siasa, basi msamiati na hata namna ya kuzungumza itakuwa ya kisiasa. Aidha, iwapo mada inayozungumziwa ni ya huzuni, au ya kuliwaza, lugha itakuwa ni ya kuliwaza na iliyojaa msamiati wa kutia moyo au kuhimiza.Mathalani, iwapo mazungumzo yanahusu mada ya kutawala, istilahi na msamiati unaoafiki mada ya utawala utateuliwa na kutamalaki katika mazungumzo. Lugha ya kisheria hutumia sentensi ndefu ndefu, marudio na istilahi maalumu za kisheria.

✍Njia za mawasiliano

Matumizi ya lugha yanaweza kuchukua njia ya mazungumzo rasmi, mazungumzo ya kawaida, mazungumzo kwa njia ya simu au maandishi.

Mawasiliano kwa njia kama hizi huweza kutofautiana. Kwa mfano, mawasiliano ya maandishi huhitaji matayarisho kabambe kuliko yale ya mazungumzo. Maandishi huhitaji muda wa kupanga mawazo, kuteua msamiati, miundo ya sentensi na kuakifishwa. Iwapo haya hayatazingatiwa, huenda mawasiliano yasitokezee barabara. Mazungumzo ya mdomo, hasa yasiyo rasmi, hayatilii maanani mambo haya sana na wakati mwingine huenda yakapuuzwa na mawasiliano yakatokea. Hii ni kwa kuwa kinyume na maandishi, mazungumzo ya mdomo yanaruhusu matumizi ya viziada lugha, kama vile kukonyeza jicho, kukunja au kukunjua uso, kutabasamu na kadhalika. Haya ni mambo yasiyowezekana katika maandishi.

✍Taaluma/ kazi

Tukichunguza matumizi ya lugha miongoni mwa wanataaluma, tutabaini upekee wake kutokana na sifa za matumizi yake. Matumizi ya lugha yatategemea taaluma husika. Istilahi hizi zinaeleweka na wale wanaoshirikiana ama wanaofanya kazi katika taaluma hizi. Kwa hivyo, kila mara wanataaluma wanapowasiliana, watatumia msamiati katika taaluma hiyo bila kutatiza mawasiliano yoyote. Ndivyo ilivyo katika fasihi ambapo istilahi fulani zinatumiwa na kueleweka katika muktadha wa taaluma hiyo. Hata hivyo, matumizi ya lugha kulingana na taaluma huwa na sifa zifuatazo:

Kuepuka matumizi ya msamiati au lugha inayoweza kuwa na fasiri nyingi na endapo litafanyika, mzungumzaji hulazimika kutoa ufafanuzi wa kounyesha maana mahsusi inayolengwa katika mazungumzo.

Matumizi ya lugha ya kitaaluma huzingatia ukweli wa mambo bila kuzua porojo, uzushi au uongo.

Aidha, hueleza mambo kimantiki, yaani kuelezea yanayozungumziwa kwa mtiririko maalumu unaoeleweka.

Katika matumizi ya lugha ya kitaaluma, kuna matumizi makubwa ya istilahi au msamiati wa taaluma husika.

Lugha hii huendesha maelezo kwa njia isioonyesha mapendeleo au hisia za mzungumzaji wake.

✍Kiwango cha elimu

Watu hutofautiana kulingana na jinsi wanavyotumia lugha kutegemea kiwango cha elimu walichonacho wahusika. Kwa mfano, wanafunzi wa shule za upili watazungumza kwa nji Fulani na kutumia msamiati ulio sawa ikilinganishwa na watakapowasiliana na wale wenzao wa shule ya msingi.Vilevile, mtaalamu wa chuo kikuu akianza kuwasiliana na mwanafunzi wa shule ya msingi atakuwa na wakati mgumu kufikiria na kuteua msamiati ambao utafaa kumweleza mwanafunzi huyo chochote atakacho kufahamu.

✍Wakati

Hii ni kaida nyingine inayodhibiti matumizi ya lugha katika jamii. Lugha ni chombo kinachotegemea mapito ya wakati. Kuna kipindi cha wakati ambapo msamiati au istilahi fulani itakuwa maarufu na itakuwa kinywani mwa kila mtu. Baadaye, matumizi ya istilahi hiyo hufifia na istilahi nyingine kuchipuka. Mathalani, katika uwanja wa kisiasa, misimu kama vile fuata nyayo, ruksa na kadhalika ilikuwa ikitumika pakubwa. Leo hii haitumiki sana kutokana na mpito wa wakati na kipindi kingine cha kisiasa. Kuna wakati noti ya shilingi mia tano ilikuwa imepewa jina Jirongo, hasa wakati wa kura za 1992. Hata hivyo, matumizi hayo nayo yalififia baada ya muda.

✍Imani za jamii

Jamii-lugha ni kundi la watu ambao huzungumza aina moja ya lugha. Kuna baadhi ya jamii ambazo huchukulia matumizi ya maneno mengine kuwa miiko ikilinganishwa na nyingine. Kwa hivyo, maneno haya huepukwa, na badala yake maneno ambayo ni safi ama msamiati usio na makali hutumiwa.

Alhamisi, 12 Desemba 2019

VIPENGELE MUHIMU KATIKA USANIFU WA MAANDISHI

USANIFU WA MAANDISHI:

🎓Usanifu wa maandishi katika fasihi ni kitendo au mchakato wa kuchambua mbinu mbalimbali za kifani/kisanaa zilizotumiwa na msanii katika kuiumba kazi yake ya fasihi.

Katika fasihi, usanifu wa maandishi huhusisha matini za aina tatu:

1.Riwaya/monolojia/masimulizi.
2. Tamthiliya/dayalojia/majibizano.
3. Ushairi (mashairi na tenzi).

🎓Mbinu za kisanaa/kifani zinazochambuliwa katika usanifu wa maandishi ni pamoja na:

A. Muundo:

👉Muundo ni mpangilio au mtiririko wa visa na matukio katika kazi ya fasihi .
👊Ikiwa matini ni Tamthiliya au riwaya , muundo waweza kuwa wa;
*moja Kwa moja (msago).
*muundo rukia/rejeshi/kioo.

✊Ikiwa matini ni Shairi, muundo hubainishwa Kwa kuangalia idadi ya mishororo(Mistari) katika beti zinazounda shairi hilo.

 Miundo katika shairi ni kama ifuatavyo:

#Tamolitha/Monolitha- muundo wa shairi ambapo ubeti hujengwa na msitari mmoja tu.
#Tathnia- Mistari miwili katika ubeti
#Tathlitha- Mistari mitatu katika ubeti
#,Tarbia- Mistari minne katika ubeti
#Takhmisa- Mistari mitano katika ubeti
#Sabilia - Mistari sita na kuendelea katika ubeti.


B:Mtindo:
👉Ni namna au jinsi msanii anavyoiumba kazi yake ili kuipa upekee kati yake na wasanii wengine. Mtindo huhusisha Matumizi ya mbinu mbalimbali katika uandishi wa kazi za fasihi kama vile:
@Matumizi ya Taarifa ya habari.
@Matumizi ya matangazo.
@Matumizi ya mabango.
@Matumizi ya Nafsi
@ Matumizi ya Barua n.k

✊Ikiwa matini ni Shairi , mtindo hubainishwa Kwa kuangalia iwapo shairi linazingatia urari wa vina na mizani (mtindo wa kimapokeo) au iwapo shairi halijazingatia urari wa vina na mizani( Mtindo wa kisasa).

C . Matumizi ya Lugha .
👉  Usanifu wa maandishi huhusisha uchambuzi wa vipengele vikuu vitatu vya lugha, ambavyo ni:

#Tamathali za semi
#Semi mabalimbali.
#Mbinu nyingine za kisanaa.

-Vipengele hivi ndivyo huifanya lugha kuonekana nyepesi au ngumu katika matini hiyo.

D. Wahusika.
👉Katika katika za fasihi wahusika waweza kuainishwa Kwa vigezo vifuatavyo:

 I: Kigezo cha Uhusika wa mhusika.
- Kwa kuzingatia kigezo hiki, kuna aina kuu mbili za wahusika:
(a). Wahusika wakuu
(b). Wahusika wadogo - Hawa wanaweza kuwa wasaidizi au wajenzi.

II: Kigezo cha Sifa /Tabia za mhusika.
- Kwa kuzingatia kigezo hiki ,kuna aina tatu za wahusika:
(a). Wahusika Duara
(b). Wahusika bapa
(c). Wahusika shinda/Foili.

✊Katika usanifu wa maandishi ni muhimu kubainisha wahusika na Uhusika wao katika matini husika.


E: Mandhari.

👉 Ni sehemu au mazingira ambamo matukio na matendo katika kazi ya fasihi hutendea au hutukia. Katika fasihi Mandhari yaweza kuwa halisi au ya kubuni.
- Ni muhimu kubainisha Mandhari katika matini husika .


🎓Mwl. Philemon Benard Masalu🎓








Alhamisi, 14 Februari 2019

Mawasiliano ya Mwl. Masalu

Philemonmasalu@gmail.com
0765671622
0678887818
Kwa msaada wowote wa Kiswahili kidato cha I hadi cha VI.

Pia tembelea blog ya *Wadau wa Kiswahili* kupitia link hii 👇👇👇
Philemon masalu.blogspot.com

DHIMA ZA Umbo la O-REJESHI ( Kiswahili kidato cha sita -Tahossa- kanda ya ziwa, 2019)

SWALI: Kwa kutumia mifano, eleza dhima tano (5) za umbo la O-rejeshi katika tungo za Kiswahili.

👉O-REJESHI ina dhima au kazi (Matumizi) zifuatazo katika tungo za Kiswahili;

✍O-rejeshi hudokeza njeo/wakati.
Mfano Juma ali-po-kwenda sisi tunaanza kula= Po  hudokeza Muda/wakati.

✍O-rejeshi hudokeza mahali(sehemu)
Mfano mahali ali-mo-lala={mo} hudokeza mahali ambapo ni ndani ya kitu
Ali-po-elekea= {Po} hudokeza mahali dhahiri.

✍O-rejeshi hudokeza namna au jinsi vitendo kilivyofanyika au mtu au kitu kilivyo.
Mfano ana-vyo- simulia (vyo)
Watoto wali-vyo- pigwa(vyo)

✍O-rejeshi hutumika kama kirejeshi, yaani kurejelea kitajwa katika umbo la kitenzi ambapo kitajwa hicho kinaweza kuwakilisha mtenda/mtendewa au mtendwa.
Mfano, Kitabu kili-cho-potea, (cho) inategemea kitabu.
Nguo zili-zo-chanika, (zo) inarejelea nguo.

✍O-rejeshi hutumika kama kiunganishi. Umbo la O-rejeshi hupachikwa katika kitenzi cha kishazi tegemezi ili kukiunga na kitenzi kikuu cha kishazi huru ambavyo kwa pamoja huunda sentensi changamano.
Mfano,
mtoto ali-ye-kuja Jana ameondoka leo. Kirejeshi ( -ye- )kinaunga vishazi viwili ambavyo ni
Mtoto alikuja Jana na Mtoto ameondoka leo.

👊Umbo la O-REJESHI hubadilika badilika kutokana na mazingira ya utokeaji au upachikwaji wake. Baadhi ya maumbo ya O-rejeshi ni pamoja Na;
 o, ye, cho, vyo, lo, po, mo, ko, zo, yo, n.k.

Mwl. Masalu©2019
Philemonmasalu.blogspot. com

MAZINGIRA YA UTOKEAJI WA O-REJESHI

Swali: Kwa kuzingatia sarufi ya lugha adhimu ya Kiswahili fafanua mazingira makuu matatu ya utokeaji wa umbo la O-rejeshi.

Dhana ya O-rejeshi
*O-rejeshi ni viangama au viambishi vinavyotumika katika tungo Kwa kurejelea mawazo,nomino au maumbo yaliyokwisha tajwa au yanayojulikana, (Saluhaya,2016).

O-rejeshi ni kiambishi kinachotumiwa kurejelea kwenye nomino ambayo huwa imetajwa kabla ya kitenzi chenyewe kutajwa. Viambishi hivi husababisha utegemezi katika sentensi, (Masebo,2016).
Mfano, watoto wadogo waliocheza vizuri wamezawadiwa.

✍Mazingira ya utokeaji wa O-REJESHI

Katika lugha adhimu ya Kiswahili umbo la O-rejeshi huwezi kutokea katika sehemu kuu tatu za neno zifuatazo;

👉Katikati ya mzizi na viambishi na viambishi awali (V.A+ O-rejeshi+ mzizi wa neno)
Mfano. Iliyopotea= i-li-yo-pote-a, hapo kirejeshi "yo" kipo katikati ya viambishi awali i-, li- na mzizi -pote-

👉Mwishoni wa kitenzi (kitenzi + O-rejeshi)
Mfano liumalo= li-um-a- lo, hivyo kirejeshi -lo-kimetokea mwishoni mwa kitenzi "Uma"

👉Kwenye mzizi wa AMBA (-Amba- + O-rejeshi)
Mfano, ambacho= -Amba- +kirejeshi "cho"
Ambaye= Amba+ kirejeshi -"ye"

👌Mbali na mazingira hayo bado umbo la O-rejeshi hujitokeza katika👉 ngeli za Kiswahili,👋 japo utokeaji wake hapa hutegemea aina ya nomino inayorejelewa.
Ni dhahiri kuwa katika ngeli umbo la O-rejeshi huundwa kwa;
i. Kipatanishi cha ngeli ya nomino(kipatinishi).
ii. Mofimu {o, au ye} ya urejeshi (kirejeshi).

Mfano katika ngeli ya YU-A/WA.
Mtoto ana-ye-soma(umoja)
Watoto wana-o-soma (Wingi)

Katika ngeli ya LI/YA
Chungwa li-lilooza(Umoja)
Machungwa ya-liyooza(Wingi).

Mwl. Masalu©2019

Philemonmasalu.blogspot.com

Masharti ya upachikaji wa O-rejeshi katika lugha ya Kiswahili.

Masharti ya upachikaji wa O-rejeshi katika lugha ya Kiswahili ni pamoja Na;

*Ni lazima kuwepo na Nomino au Kiwakilishi kinachorejelewa katika mazungumzo baada ya kuwa kimetajwa wazi. Mfano: mtoto aliyeiba

*Utokeaji wa O-rejeshi mwishoni mwa kitenzi huruhusu kitenzi hicho hubeba kiambishi cha wakati .mfano pale tuchezapo

*Mara baada ya kupachika O -rejeshi katika mzizi wa "Amba" kitenzi kinachofuata hakitapata athari za moja Kwa moja za O-rejeshi.
Mfano. Mkono ambao umevunjika. Hivyo kitenzi umevunjika hakijathiriwa na kirejeshi kilichopachikwa katika mzizi -Amba-.

*Katika ngeli ya kwanza umoja (Kwa kigezo cha kisintaksia), yaani ngeli ya Yu-A/WA; O-rejeshi lazima iwe "Ye" ambayo hubeba nafasi. Mfano. Mtoto aliyepotea.

*Ni lazima kuwepo na upatanishi wa kisarufi kati ya kipashio cha urejeshi na Nomino inayorejelewa. Mfano, Kiti kilichonunuliwa kimevunjika.
Kirejeshi -cho- kinapatana na Nomino kiti.

Mwl. Masalu©2019
philemonmasalu.blogspot.com
*

Maendeleo ya Kiswahili

KISWAHILI: HISTORIA NA MAENDELEO
1. Kiswahili kabla ya Ukoloni
Historia ya lugha ya Kiswahili imeanza kabla ya miaka ya 1000 BK kwenye pwani ya Afrika Mashariki. Kuenea kwake kabla ya ukoloni kulisababishwa na shughuli zakibiashara miongoni mwa Waafrika. Biashara hii, ilikuwa imeshamiri sana katika upwa wote wa Afrika Mashariki. Wenyeji wa maeneo haya, walikuwa na mawasiliano ya muda mrefu kabla ya kufika kwa wageni wa Kiarabu na Kizungu. Kulikuwa na safari zakibiashara baina ya pwani na bara zilizokuwa zikifanywa na Waafrika wenyewe. Katika safari hizo, watu wa bara waliofika pwani walijifunza na walikitumia Kiswahili cha pwani na kukieneza waliporejea kwao. Hao ndio walioanza, bila kukusudia, kuieneza lugha ya Kiswahili kutoka pwani hadi sehemu za bara. Waswahili waliendeleza misafara ya kibiashara hadi nchini Kongo na maeneo mengine ya Afrika ya Kati.
2. Kiswahili katika kipindi cha Ukoloni
Wageni walioshirikiana na wenyeji katika kueneza Kiswahili Afrika Mashariki wakati wa ukoloni ni Waarabu, Waajemi, Wareno, Wajerumani na Waingereza. Sababu zilizowafanya wageni hawa waje Afrika Mashariki ni kufanya biashara, kueneza dini nakutawala. Katika karne ya 19 BK wakoloni walifika katika bandari za pwani wakatumia mara nyingi makarani, askari na watumishi kutoka eneo la pwani na kujenga vituo vyao bara. Watu hawa walisaidia kukipeleka Kiswahili katika pande za bara. Kiswahilikilikuwa lugha ya utawala katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Wakoloni walitumia kazi za Wamisionari wa awali hasa Ludwig Krapf aliyewahi kufanya utafiti wa lugha na kutunga kamusi na sarufi za kwanza pamoja na kuleta mfumo wa kuandikaKiswahili kwa herufi za Kilatini.
Kukua kwa lugha ya Kiswahili kulikosababishwa na shughuli za kiutawala na kibiashara kulisababisha kuingia kwa maneno mengi mapya katika Kiswahili.Kiswahili kimeonyesha uwezo mkubwa wa kupokea maneno kutoka lugha tofauti kikitumia maneno haya kufuatana na sarufi ya lugha za Kibantu. Kwa jumla Kiswahili kina maneno mengi yenye asili ya Kiarabu ambayo inakadiriwa kuwa kati ya 30% na 40%. Hali hii ni kutokana na uhusiano ya muda mrefu baina ya pande hizi mbili na pia kutokana na lugha hii kuwekwa kwenye maandishi kwa kutumia herufi za Kiarabu tangu karne ya 13 BK. Hata hivyo, Kiswahili ni lugha yenye asili ya Kibantu kwa kutumia hoja za kiisimu na kihistoria.
Wafanyakazi kutoka makabila mbalimbali katika ujenzi wa reli, ufanyaji kazi katika mashamba makubwa yaliyozalisha mazao ya biashara, na katika migodi watu wa makabila mengi walitumia Kiswahili. Kwa namna hiyo lugha ya Kiswahili ilienea zaidi. Ili kuendesha shughuli zake, serikali ya kikoloni ya Waingereza iliona haja ya kuwa na lugha moja ambayo ingetumika katika makoloni yao yote ya Afrika Mashariki. Hata hivyo lugha ya Kiswahili ilikuwa na lahaja nyingi sana zilizoenea katika mwambao wote wa Afrika Mashariki na baadhi ya sehemu za bara. Kulikuwa na haja ya kuwa na lahaja moja ambayo ndiyo ingefanywa lugha rasmi.
Ili kukidhi haja hiyo, kamati maalumu ya kushughulikia suala hilo iliyojulikana kama kamati ya lugha ya Afrika Mashariki iliundwa. Mwaka 1929 Katibu wa halimashauri ya magavana wa Afrika Mashariki aliziandikia serikali nne kuhusu suala la kuanzishwa kwa kamati ya lugha ya serikali zote nne na tarehe 1-1-1930 kukaanzishwa kamati iliyoitwaInter-Territorial Language (Swahili) Committee ili ihusike na kusanifisha Kiswahili. Kamati hii iliiteua lahaja ya Kiunguja kuwa msingi wa lugha rasmi yamaandishi. Suala hili lifuatiwa na uchapishaji wa kamusi na vitabu vya sarufi.
3. Nafasi ya Kiswahili Duniani
Kiswahili sanifu siyo tena lahaja ya Kiunguja kama ilivyochukuliwa kitambo, bali ni lugha rasmi ya Kiswahili inayotumiwa na watu wengi sana Afrika Mashariki na Kati. Kiswahili sanifu kina msamiati na istilahi za taaluma mbalimbali. Kimeandikiwa kwamapana na kinatumika na watu mbalimbali katika sehemu nyingi za dunia. Lugha hii ina uwezo mkubwa sana wa kukabiliana na mazingira mapana zaidi na mabadiliko ya kisayansi na kiteknolojia. Nchi za Afrika ya Mashariki, hasa Kenya, Uganda na Tanzania ni nchi ambazo zimekuwa na uhusiano wa karibu tangu zamani. Zimekuwa na ushirikiano kihistoria na zote zilitawaliwa na Uingereza, hali iliyosaidia kuanzishwakwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wakati wa uhuru. Lugha hii imekuwa ya watu wengi mijini na vijijini hasa Tanzania na Kenya. Kiswahili kinatumika pia Kaskazini mwa Msumbiji, Somalia, Kongo, Rwanda, Burundi, Sudani, na maeneo ya Malawi na Zambia.
Leo, lugha hii ina umuhimu mkubwa kwa sababu ya kuenea na kukusanya watu wa makabila na nchi kadha wa kadha wakaweza kufahamiana kwa lugha moja. Pia imekuwa ikitumiwa katika kusambaza habari katika vituo na mashirika mbalimbali vyahabari duniani. Kuna taasisi zinazolenga kukuza na kuimarisha Kiswahili kama vile Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) nchini Tanzania, Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), nchini Kenya kuna Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA). Pia kuna Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na idara za Kiswahili katika vyuo vikuu mbalimbali vya Tanzania, Kenya naUganda na vyuo vikuu vingi duniani.
3.1. Afrika Mashariki
Baraza la Kiswahili la Taifa BAKITA (Tanzania), Chama cha Kiswahili cha Taifa CHAKITA (Kenya) na wawakilishi kutoka Uganda walianzisha wazo la kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la Afrika Mashariki. Wazo hili liliongoza katika kuanzisha Kamisheni ya Lugha ya Kiswahili ambayo ilianza mwaka 2012. Hii ni kwa sababu Kiswahili ndiyo lugha ya Afrika Mashariki yenye uwezo wa kuwaunganisha watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inasimamia ukuzaji na maendeleo ya matumizi ya Kiswahili kwa ajili ya umoja wakikanda pamoja na maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi zote. Lengo lake ni kukuza Kiswahili kiwe lugha ya matumizi mapana katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ushirikiano wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umeiwezesha lugha hii kukua na kusambaa sehemu kubwa ya ukanda huu. Pamoja na hayo, hadhiya Kiswahili inapanda na kukua kwani kinatumika katika mikutano mingi zaidi ya Kimataifa kama ilivyo sasa katika Umoja wa Afrika.
3.1.1 Tanzania: Nchini Tanzania, Kiswahili ni lugha ya taifa; lugha rasmi katika shughuli za serikali na bunge, lugha inayotumika kufundishia Shule za Msingi nakama somo katika elimu ya juu. Hata hivyo, sera ya elimu ya 2015 (tamko la 3.2.19) imeidhinisha rasmi matumizi ya Kiswahili katika mfumo wote wa elimu kuanzia Shule za Msingi hadi Vyuo Vikuu. Kiswahili kinatumika kutoa mafundisho ya dini makanisani na misikitini. Kiswahili ni lugha kuu inayotumika katika vyombo vya habari kama vile televisheni, redio na katika idadi kubwa ya magazeti ikiwemo mitandao mbalimbali ya kijamii.
3.1.1.1 Kiswahili na harakati za ukombozi Tanzania
Kiswahili kilitumika kama lugha ya mawasiliano katika harakati za siasa za kudai uhuru; mathalani mikutano ya vyama vya siasa kama vile ya Tanganyika African Association (TAA) iliendeshwa kwa lugha ya Kiswahili. Aidha, matumizi ya lugha ya Kiswahilikatika harakati hizi yalipanuka zaidi wakati wa kuundwa kwa chama cha siasa cha TANU 1954, ambacho viongozi wake akiwemo Mwalimu Julius Nyerere walihutubia wanachama wa chama hicho kwa Kiswahili. Safari za viongozi za kuzunguka Tanganyika nzima ili kuhamasisha Watanganyika kuunga mkono harakati za kudai uhuru zilifanywa kwa lugha ya Kiswahili. Jambo hili lililofanya Kiswahili kienee nakipate mashiko nchini Tanganyika. Pia, nyimbo za siasa zilizotungwa kuhamasisha wananchi zilikuwa za lugha ya Kiswahili na kukipa Kiswahili dhima mpya ya kuwa alama ya Umoja, Uzalendo, Utanganyika na Uhuru.
3.1.2 Kenya: Nchini Kenya Kiswahili ni lugha ya taifa.Katiba ya Kenya ya ( 2000) Ibara ya 7(1) imekipa Kiswahili sura mpya ya kuwa lugha rasmi na lugha ya taifaKiswahili hufundishwa na kutahiniwa shuleni na vyuoni. Lugha hii inayotumika bungeni na katika kuendesha biashara. Kiswahili ni lugha kuu ya mawasiliano wanapokutana watu wa makabila tofauti. Kiswahili kinatumika katika jeshi na polisi. Ni lugha ya kuendesha kampeni za kisiasa mijini na vijijini. Kiswahili kinatumika katika kuendesha ibada makanisani na miskitini. Vyombo vya habari vinavyotumia Kiswahili nchini Kenya bado ni vingi, kinatumika katika programu kadhaa redioni na kwenye televisheni. Aidha nchini Kenya Kiswahili kinatumiwa sana katika mawasiliano ya mitandao ya kijamii na blogu za watu binafsi.
Tume mbalimbali za elimu nchini Kenya ikiwemo Tume ya Mackay, Tume ya Wamalwa, Tume ya Gacathi miongoni mwa tume nyingine zilipendekeza Kiswahilikitumiwe katika ngazi mbalimbali za elimu. Haya yalifanya Kiswahili kushika kasi nchini Kenya. Aidha marais wa kwanza wa Kenya wote walitilia maana matumizi ya Kiswahili kote nchini.
Kiswahili pia kilitumika kama chombo cha umoja miongoni mwa wakenya na moja ya nyenzo ya kuunganisha watu katika harakati za kudai uhuru.
3.1.3 Uganda: Kiswahili kimeanza kutumika kwa mapana na marefu kutoka 2005. Kiswahili kinafundishwa na kutahiniwa katika viwango mbalimbali vya elimu. Aidha, Chuo kikuu cha Makerere kina Idara ya Kiswahili ambayo hufundisha isimu na fasihi kwa Kiswahili. Kiswahili kimekuwa ndiyo lugha ya mawasiliano ikitumiwa zaidi na askari na pia katika kufanya mawasiliano na wageni kutoka katika nchi jirani za Afrika mashariki.
Kiswahili kinatumika sana katika shughuli za biashara na mawasiliano ya kawaida nchini Uganda.
Kuna waandishi wa vitabu vya Kiswahili na pia wanamuziki nchini Uganda ambao wanatunga nyimbo kwa lugha ya Kiswahili
3.1.4 Burundi: Kiswahili kinatumika sana mashariki ya Burundi. Kiswahili kinafundishwa katika baadhi ya vyuo m.f. chuo cha wanajeshi cha Bujumbura na katikaChuo Kikuu cha Bujumbura. Aidha, Kiswahili hufundishwa katika taasisi za mabwana fedha na taasisi ya mawasiliano ya simu. Kiswahili hutumika pia katika Redio Burundi, Ibyizigiro, Isanganiro na katika televisheni kwa baadhi ya vipindi vyake kama vilehabari, matangazo, vipindi vya utamaduni na mafunzo, na matangazo ya mpira.
3.1.5 Rwanda: Kiswahili kinatumika sokoni na mijini. Lugha ya Kiswahili inafundishwa katika chuo kikuu cha Rwanda. Wapo baadhi ya wananchi wanaojiandikisha kujifunza Kiswahili katika madarasa ya jioni. Rwanda imeanzisha Kiswahili katika mtaala wa taifa na kuongezwa katika orodha ya lugha rasmi. Redio Rwanda kuanzia mwaka 1961 imekuwa na programu za Kiswahili kama vile taarifa ya habari, matangazo ya mpira na salamu za wasikilizaji.
3.2 Nafasi ya Kiswahili katika Nchi nyingine za Afrika
3.2.1 Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo: Kiswahili ni miongoni mwa lugha nne za kitaifa zinazotumiwa nchini humo ikiwa ni pamoja na Kilingala, Kiluba na Kikongo. Kiswahili kimeenea zaidi mashariki mwa nchi hiyo ambako kilifika kutokana na misafara ya biashara ya kutoka Zanzibar na Pwani ya Tanganyika.
3.2.2 Msumbiji: Kiswahili kinatumika kaskazini mwa msumbiji. Katika Chuo cha Mambo ya Afrika ya Kusini hutangaza katika Kiswahili baadhi ya vipindi vyao vya redio
3.2.3 Visiwa vya Komoro: Kiswahili hutumika katika badhi ya vipindi vya redio.
3.2.4 Ghana: Kiswahili kinatumiwa na taasisi k.v. Shirika la Utangazaji la Ghana, Taasisi ya Elimu ya Ghana na Chuo Kikuu cha Ghana.
3.2.5 Zambia: Sehemu za Zambia zilizo mpakani na Tanzania hutumia Kiswahili
3.2.6 Somalia: Kiswahili kinatumika Kusini mwa Somalia lakini hivi karibuni kimeanza kuenea kwingi na kwa haraka sana. Hii ni kutokana na maingiliano ya biashara.
3.2.7 Malawi: Kuna wasemaji kadhaa huko kaskazini mwa Malawi
3.2.8 Afrika Kusini: Chuo kikuu cha Kwazulu Natal kimeanzisha masomo ya BAKiswahili.
3.2.9 Zimbabwe: Lugha ya Kiswahili imepangwa kuwa moja kati ya lugha nne za
kigeni za lazima katika mtaala wa elimu .
3.2.10 Libya: Ni moja kati ya nchi za Afrika iliyo nje ya Afrika Mashariki ambayo imekuwa ikiendeleza Kiswahili kwa muda mrefu kwa kufundisha Kiswahili katika moja ya vyuo vyake vikuu vikongwe, chuo kikuu cha Sebha katika Idara ya Lugha na Stadi za Afrika.
3.3 Kiswahili katika sehemu nyingine za Dunia
Lugha ya Kiswahili imekuwa na umuhimu mkubwa duniani kwa ujumla. Matumizi yake kimataifa ni kama ifuatavyo:
1. Mikutano ya Kimataifa:
· Kiswahili kinatumika kama lugha ya kazi katika vikao vya Umoja wa Nchi za Afrika (AU) kutoka 2004. Uteuzi wa Kiswahili kuwa lugha ya kazi ulitokana na sababu kwamba hakukuwepo na lugha nyingine za Afrika zinazokidhi viwango vya kimataifa.
· Umoja wa Nchi huru za Afrika (OAU) uliteua Kiswahili kama moja ya lugha za Kiafrika inayotumiwa katika mikutano yake. Uteuzi wake ulitokana na kikao cha Mawaziri wa Utamaduni 1988. Mawaziri walitoa wazo la kuwa na lugha moja ya Kiafrika itakayotumika pamoja na lugha za kigeni kama vile Kiingereza, Kireno, Kifaransa na Kiarabu. Pendekezo la Mawaziri wa Utamaduni la kukifanya Kiswahili kuwa ni lugha ya Kiafrika na ya tano katika vikao vya OAU ni uamuzi mzuri ambao umekipa Kiswahili hadhi kubwakimataifa. Pendekezo hilo liliridhiwa na wakuu wa nchi katika mkutano wao huko Addis Ababa Ethiopia.
· Kiswahili kimekubaliwa kutumika katika mikutano ya UNESCO mradi tu kuwepo na mkalimani.
1. Idhaa za Kimataifa: Kuna vituo vya redio kutoka nchi mbalimbali duniani ambavyo hurusha matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili. Mfano wa idhaa hizo ni kama vile Sauti ya Amerika (Marekani), BBC (Uingereza), Redio Deutche Welle (Ujerumani), Redio France International (Ufaransa), China Radio Inaternational (Uchina), Idhaa ya Kiswahili Redio Japan (Japan), Idhaa ya Kiswahili redio Tehran, Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya Umoja wa Mataifa, Idhaa ya Kiswahili ya Redio Cairo (Misri), Idhaa ya Kiswahili Iran, Redio Sudani, Redio Vatican, Redio India, Redio ya Korea Kusini, Redio Moscow Inaternational (Urusi).
2. Vyuo vinavyofundisha Kiswahili: Duniani kuna nchi mbalimbali ambazo zimeanzisha programu ya somo la Kiswahili katika vyuo vyake vikuuu au kwenye taasisi zake za lugha za kigeni. Miongoni mwake ni:
(i) Marekani: Kuna vyuo na vituo mbalimbali vinavyofundisha Kiswahili ikiwa ni pamoja na: Chuo Kikuu cha Boston (The African Studies Centre), Chuo Kikuu cha Cornel (Cornell University’s AfricanaStudies and Research Centre), Chuo Kikuu cha Havard (Departiment of African and African American Studies), Chuo Kikuu cha Howard (African Studies Departiment), Chuo Kikuu cha Indiana, Chuo Kikuu cha Michigan, Chuo Kikuu cha Ohio (African –American and AfricanStudies), Chuo Kikuu cha Ohio (Centre for African Studies), Chuo Kikuu cha Stanford, Chuo Kikuu cha Wiscounsin – Madison, Chuo Kikuu cha Pennslvania (Kituo cha Stadi za Lugha za Kiafrika), Chuo Kikuu cha Ilinois (Kituo cha Stadi za Lugha za Kiafrika).
(ii) Uchina: Kuna vyuo vikuu vitatu nchini Uchina vinavyofundisha Kiswahili ambavyo ni chuo kikuu cha mawasiliano ya habari cha China, Chuo kikuuu cha lugha za kigeni cha Beijing na chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Tianjin.
(iii) Ujerumani: Vyuo vikuu vinavyofundisha Kiswahili ni pamoja na Humburg, Berlin, Cologne na Leipzig.
(iv) Uingereza: Kiswahili kinafundishwa katika Chuo Kikuu cha London (School of Oriental African Studies- SOAS).
(v) Korea Kaskazini: Kiswahili kinafundishwa Chuo Kikuu cha Hankuk.
(vi) Japani: Kiswahili kinafundishwa katika Chuo kikuu cha Osaka.
(vii) Ufaransa: Chuo cha INALCO
3. Programu mbalimbali za kompyuta zinazotumia Lugha ya Kiswahili ni pamoja na LINUX operating System, Jambo OpenOffice, Kiolesura Fungasha Kiswahili cha Windows XP, SALAMA ( Swahili Language Manager Program).
4. Mitandao ya simu kama vile Tigo, Vodacom, Airtel, Zantel kwa Tanzania na Safaricom, Orange, Airtel na Yu kwa Kenya inatumia pia Kiswahili.
5. Kiswahili katika uga wa sanaa: Baadhi ya wanamuziki wa kimataifa wametumia maneno ya Kiswahili katika kupeleka ujumbe wa nyimbo zao ikiwa ni pamoja na: marehemu Michael Jackson (Liberian Girl). Lionel Richie, Miriam Makeba (Afrika Kusini), Helmut Lotti (Ubelgiji), Harry Belafonte (Marekani), Rocco Granata (Italia), Peter Seeger (Marekani)miongoni mwa wengine wengi.
6. Kiswahili katika tasnia ya filamu za kimataifa, baadhi ya filamu zinazolenga kutoa maudhui kuhusu Afrika zimekuwa zikitumia maneno kadhaa ya Kiswahili m.f. filamu ya Disney (The Lion king) kuna maneno k.v simba, hakuna matata na rafiki.
7. Kiswahili pia kinatumika kwa wingi sana katika mitandao ya kisasa ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram, Linkedin na Whatsup. Hali hii inakifanya Kiswahili kuenea kwa kasi mno kote duniani.

Longhorn publishers limited (2016),Kamusi Kuu ya Kiswahili.

Philemonmasalu.blogspot.com

Alama za Uakifishaji

Alama za uakifishaji
Alama za uakifishaji hutumiwa katika uandishi ili kuiweka bayana sentensi, neno au kazi nzima husika. Ili kuafikia mawasiliano mwafaka, ni muhimu kutumia alama za uakifishaji kwa njia sahihi. Baadhi ya alama za uakifishaji ni kama zifuatazo:
Na
Alama
Jina la alama
Matumizi
Mfano
1.
.
Nukta/kituo
Hutumiwa mwishoni mwatungo au sentensi.
Waliokuja jana wasogee mbele.
Hutumika katika uandishi wa vifupisho.
Dkt. = Daktari, n.k. = na kadhalika, k.v. = kama vile, prof. = profesa
Hutumika katika uandishi wa tarehe na namba zadesimali.
3.4.2015,
3.42
Hutumika mwishoni mwa orodha ya vitu.
Wanachapisha vitabuvya hisabati, historia,kiswahili, sayansi najiografia.
2.
,
Koma/mkato
Hutumika kuonyeshapumziko dogo katikasentensi.
Alipofika tu akamwita mtoto,lakini hakuitika.
Hutumika kutenganisha vitu vilivyoorodheshwa.
Alinunua papai,machungwa, maembe, ndizi na mapera.
3.
:
Nuktapacha
Kuunganisha vishazi huru viwili.
Watoto wanacheza:wakubwa wanafanya kazi
Kutenganisha dakika na sekunde.
Tuliwasili saa 2.30:29.
Kuonyesha vituvinavyotajwa kuwa viko katika orodha.
Katika ziara yakeatatembelea nchizifuatazo: Kenya,Uganda, Tanzania,Somalia na Ethiopia.
Kutenganisha Mada kuu na ndogo.
Historia ya Lugha: Kukua na kuenea kwake.
Kutenganisha juzuu na kurasa au mlango na mstari katika vitabu
Juzuu la 1: 2
Math. 5: 3-7
4.
!
Alama yakushangaa/mshangao
Baada ya maelezo ya kushangaza, kusisitiza, kushitua, kubeza au wito
Jamani! Amekufa.
Alidondoka puu!
Amina! Abee!
5.
?
Alama ya kuuliza
Hutumika katika maneno au tungo zinazoulizamaswali.
Kwa nini gharama yaumeme imepanda?
Kuonyesha neno autungo ya kushangaza nahuku ikiwa ni swali.
Hivi jana ulikutwa ofisini usiku?
6.
;
Nuktamkato
Kuunganisha dhana mbili katika sentesi ambatano.
Mshahara wa dhambi ni mauti; karama ya Mungu ni uzima wa milele.
Hutumika kabla ya kutaja maneno ambayo niviunganishi tegemezi.
Walipewa huduma zote muhimu; hata hivyo, waliamua kutoroka.
Hutumika kutenganisha vitu vilivyopo katikaorodha
Mkitaka kupita Kiswahili someni; kamusi, vitbu vyamashairi, riwaya
7.
( )
Parandesi
Hutumika kufungiamaelezo ya ziada katika tungo.
Matunda yote (maembe, ndizi na papai) yaliletwamezani.
Kuonyesha maelezo au mawazo ya mwandishiasiyekuwa mhusikakatika mchezo wakuigiza.
Alisafiri siku nyingi(takribani 25) jangwani
Kutenganisha namba au herufi zinazoorodheshavitu kwa idadi.
(1), (2), (3), (4)
(a), (b), (ch), (d)
8.
“ ”
Alama zaKunukuu (nukuu za alama moja)
Hutumika kuonyesha usemi ulionukuliwa
Baada ya mgomo, walimu walisema "Tutarejea darasani.”
Kutaja majina rasmi au yasiyo rasmi katika tungo.
Alipoingia “kigogo” tuwote walisimama.
‘ ’
9.
Nukta katishi/alama zadukuduku
Huonyesha katikasentensi iliyoandikwa kuna baadhi ya manenoyamekatishwa.
Samaki mkunje, …
Ukiona vyaelea, …
Huonyesha maelezoyanayotolewa yanavutwa
Kwenye mstari …, kaatayari…,
Nenda… .
HUtumiwa kuonyesha sentensi isiyokamilika
Kama hizi ndizo siasa za kisasa, mimi...
10.
Alama ya kistari
Hutumika kuongezamaelezo ya ziada katika sentensi.
Mwalimu wetu – wahisabati- alitufundisha vizuri sana
Hutumika badala yanuktapacha kuonyeshamahojiano
Mzazi- Ulirejea saangapi?
Mtoto – Saa moja jioni.
Hutumika pamoja na alama za nukta pacha kuonyesha vitu vilivyoko katika orodha.
Walichangia vitu vingi: mavazi, vyakula, dawa na fedha
11.
Ritifaa
Huonyesha utamkaji wa nazali au ving’ong’o
Ng’arisha, ng’ata, ng’oa, ng’atuka
Huonyesha sehemuya neno au nambailiyoachwa kwa ajili ya kufupisha
’80 = 1980
U’shakula = umeshakula
12.
*
Kinyota
Huonyesha kuwa neno au sehemu ya maandishiiliyowekewa kinyota ina maelezo zaidi.
Tasfida* ilitumika sana kwa sababu kulikuwa na watoto.
*tasfida ni maelezoau maneno ya stahayasiyokuwa na matusi au ukosefu wa adabu.
Hutumika kamanuktakatishi kwakuonyesha kuwamaneno yanayokatishwayanahitaji tasfida.
Waliendekea namazungumzo, maramlango ukafungwa *** Sauti za kutisha.
13.
{ }
Mabanomawimbi/mabanodabali
Kubainisha orodha ya vitu vyenye sifa au vya kundi moja
Seti ya namba zakuhesabia: {0, 1, 2, 3, 4, 5...9}
14.
[ ]
Mabano mraba
Kubainisha maelezoya nyongeza ya matini chanzi
Alitumia msumenomashine [powersaw]kuvunja mlango
15.
( )
Parandesi
i) Kubainisha miundotegemezi katika tungo.
ii) Kubainisha orodha ya vipengele katika sentensi.
Mgeni (aliyekuja jana) ameondoka.
Nenda kalime haraka
Nenda (Nomino)
Kalime (Kitenzi)
Haraka (Kielezi)
16.
/
Mtoi
i) Alama hii inatumikabadala ya neno "au"
wanawake/wanaume
ii) Kutenganisha vitu viwili vyenye kazimoja
kit.ele/sic. = kitenzielekezi
iii) Husimama badala ya neno 'kwa'.
km 80/saa = kilometa sitini kwa saa moja
iv) Kubainishamatamshi
/m'tai/