Alhamisi, 14 Februari 2019

Oktoba kumi na nne!

"OKTOBA KUMI NA NNE"

Oktoba kumi Na nne,
Siku siitamani Mie,
Hunifanya nilie,
Kila nikikumbuka,
Hayati Mwalimu!

Kipaza sauti kilipotangaza,
Sikuweza kuamini,
Baba kumpoteza,
Akili ilizizima,
Na mji vilio kutanda,
Katuacha mwalimu!

Mazishi yalipoisha,
Nia mimi nikaiweka,
Kumuenzi mwalimu,
Kwa yake Kalamu,
Iliyotufundisha ufahamu,
Hayati mwalimu!

Ndugu zangu nao nia moja,
Kwa pamoja walinia,
Mwalimu ndio msingi,
Wa kuijenga nyumba,

Lo! Kumbe Nia yao usoni,
 wapishi Na wanazuoni,
Kuyajenga yao matumbo,
Hakika! Kufa kufaana,
Ndivyo wanavyosema.
Takukumbuka mwalimu!

Miaka kumi sita kujongea,
Mjomba kaingia,
Jikoni kupashikilia,
Chakula kukipakua,
Kwa usawa tupate tumia,
Kumbe wengine waumia,
Na kelele kuzipiga,
Hatuhitaji busara za marehemu,
Nyumba hii kuienedesha,
Lakini mjomba yake Nia,
Kalamu ya mwalimu kuidumisha!

Nyumba kupendeza,
Wageni kututembelea,
Kwa juhudi za mjomba,
Mimi Na wenzangu,
Heshima tumepata,
Kwa kupunguza ukata,
Na elimu nayo twapata!

Tumkumbuke mwalimu!
Kwa vyetu vyema vitendo!
Sio kuendeleza magendo,
Maana nyumba twaibomoa,
Oktoba kumi na nne,
Chachu ya kukarabati,
yetu nyumba iwe thabiti,
Tumuenzini mwalimu!
                 

                Na
Mwl. Philemon masalu
Philemonmasalu@gmail.com







Shairi

Itika wito kataa maneno!

Asubuhi Na mapema,
Tarehe siwezi sema,
Ila nachoweza tema,
Siku moja mapema,
Dubu kikao kaitisha,
Na maagizo kutoa,
Swala Na sungura,
Sharti kutekeleza!

Sisi sote tu wanyama,
Tena tu jike Na dume,
Ila dubu atutaka,
Uhuru tudumishe,
Na haki ya kila mnyama,
Sharti kutekeleza!

Swala nikuulize,
Na nyie mnijuze,
Je, Unawezaa,
 Na jike mwenzio?
Au kufunga ndoa,
 Na dume mwenzio?
Kwetu sungura hilo mwiko!
Ila dubu kasema,
Sharti kutekeleza!

Marafiki Hawa wawili,
Sasa hawalali,
Mchana usiku kufikiri,
Wasipotekeleza,
wapi msaada kupata?
Maana dubu ndio kimbilio lao,
Na uombaomba ndio maisha yao,
Sauti ya dubu daima waikumbuka,
Sharti kutekeleza!

Baada ya kufikiri,
Sungura akata shauri,
Sharti hatutekelezi!
Kwani nyumba yetu nzuri,
Na chakula chetu kizuri,
Wenyewe chatutosha,
Misaada toka kwake mwisho,
tutashirikiana kufanya kazi,
Tuweze kujitegemea,
Na dubu asitutishe ,
Nasi tuna yetu malazi.

Sungura na swala wakaachana,
Kila mmoja kwake kuelekea,
Mwezi mmoja baadae,
Sungura apata kadi ya mwaliko,
Mwaliko wa harusi,
Toka Kwa swala,
Toba! Ngosha Na mbunde,
Nao wote wanaume,
Ni yao ndoa,
Mbunde ndani ya Shela,
Naye ngosha yake suti.
Tamaduni wameizika!
Swali je, Nani atazaa kati yao?
Kubali wito kataa maneno!
(01/01/2019)

Mwl. Philemon Masalu
Philemonmasalu@gmail.com





Jumatano, 13 Februari 2019

Shairi



WATOTO YATIMA!

Paukwa Pakawa...,
Miaka ikasonga,
Balaa kutokea,
Ndugu kumkosa,
Kipenzi chao baba,
Alowajali wana.
Ama kweli ni ya maulana!

Mabula Na limbu,
Sasa walaani mbingu,
Kwa mpango wa Mungu,
Wao Sasa Yatima,
Je, Kwanini sisi?
Ndicho kilio cha ndugu,
Kwa huzuni Na uchungu.

Kama ilivyo ada,
Kifo ndio mada,
Lakini kupita muda,
Majonzi yakakimbia,
Na maisha kwendelea,

Mjane anza tapatapa,
Mume mwingine apata,
Watoto wamkumbuka,
Wao kipenzi baba,
Kwa mateso wanopata,
Wote waazimu,
urithi wao kutaka,

Ba' wa kambo tatizo,
Kila kukicha mizozo,
Mithili ya wachuuzi Kwa soko,
Mara hii nzima ile uozo,
Baba huyu kikwazo,
Maisha yetu mateso,
Ila wimbo wake mezani,
Wanangu tuishi Kwa amani.

Jambo lilo baya,
 Sasa watoto Hali mbaya,
Ba' wa kambo haoni haya,
Mali zote zake,
Mabula Na limbu wasema haya!
Na Dua zao si mbaya,
Muda ukiwadia,
Nasi tutapoteza haya,
Kudai kilicho chetu,
Fahari ya nyumba yetu!

                   Na
Mwl. Philemon Masalu
Philemonmasalu@gmail.com.





Shairi la Ukoko

Ukoko ama kweli ukoko,
U mtamu uulapo,
Kama nyama ya kiboko,
Lakini shida yake ukoko,
Ni huku kuliwa mwishoni!
 
Wengine ukoko waula,
Wakiwa wima,
Mithili ya wapiga kura,
Msitarini kumpitisha mgombea,

Walaji wagombana,
Ukoko chanzo cha uhasama,
Kila siku wasutana,
Mara o we wala sana!
Achia nasi tule!


Utamu wa ukoko,
Wamponza koo,
Kisu Kwa Shingo,
Pasi jasho la mbio,
Ukoko chanzo cha mapigo.
13/10/2018).





FASIHI NA JAMII

Swali.
Jadili ni Kwa namna gani fasihi na jamii huhusiana huku ukijikita katika fasihi ya Kiswahili.